Huduma ya majisafi

Vyanzo vikuu vya maji kwa wakazi wa Jiji la Tanga ni Bwawa la Mabayani lililopo kijiji cha Mabayani kilomita 26 kutoka Tanga Mjini na kisima cha Mwakileo. Kisima cha Mwakileo kina uwezo wa kuzalisha 3,120m3/siku wakati Bwawa la Mabayani lina uwezo wa kuhifadhi maji wa mita za ujazo milioni 7.7. Hifadhi hii imejengwa kuvuka Mto Zigi unaotiririka kutoka Milima ya Usambara inayolishwa na eneo la vyanzo vya maji la 895sq.km. Mazingira ya hifadhi yamezungukwa na uoto wa asili wa nyasi na miti inayofunika eneo la 233.8Ha.
Vyanzo vya maji kwa wakazi wa Mji wa Muheza ni Mto Mkulumuzi wenye kidakio kilichopo kwenye vilima vya Magoroto umbali wa kilomita 11.5 kutoka Muheza Mjini na Visima sita vilivyopo katika maeneo mbalimbali ndani ya kata sita (6) za eneo la mamlaka ambazo ni Genge, Majengo, Kwemkabala, Masuguru, Mbaramo na Tanganyika. . Uwezo wa uzalishaji ni wa kidakio 1,425m3/siku wakati Visima sita vinazalisha maji kwa wastani wa 357.6m3/siku.
Wakazi wa Mji wa Pangani wao wanategemea Visima vitatu vinavyofanya kazi kati ya visima sita. Visima hivyo viko eneo la Boza katika Kata ya Kimang’a kilomita 4 kutoka Pangani Mjini. Visima hivyo vina uwezo wa kuzalisha maji kwa wastani wa 939m3/siku.