Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga inaendesha na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019, Mikataba ya Utendaji Kazi na Wizara ya Maji na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011, Miongozo ya Uendeshaji, Sheria ya EWURA SURA 414 ya mwaka 2001 na Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002.
Mamlaka ilianza shughuli zake Julai 1998 kwa utoaji huduma katika Jiji la Tanga na kufuatia maagizo ya Serikali mwezi Septemba, 2019 kupitia GN 666 miji ya Muheza na Pangani. Majukumu makubwa ya Tanga UWASA ni kusambaza maji ya kutosha, safi na salama ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakazi wa Jiji la Tanga, Miji ya Muheza na Pangani na uondoshaji majitaka kwa usalama kwa kuzingatia viwango vya mazingira na afya.
Ikiwa na dhima ya kuwa shirika la kimataifa linalomjali mteja wa huduma ya maji safi na maji taka, dhamira ya Mamlaka ni kutoa huduma ya maji safi na salama ya kutosha na bora kwa wakazi wa Jiji la Tanga, Miji ya Muheza na Pangani kupitia watumishi wenye ari na umakini kwa wateja katika mazingira. rafiki.