Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

MAMLAKA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA TANGA

(Tanga UWASA)

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
/ News

VEi - Tanga UWASA YAZINDUA MAJI CLUB MKWAKWANI SEKONDARI

Imewekwa: 01 October, 2026
VEi - Tanga UWASA YAZINDUA MAJI CLUB MKWAKWANI SEKONDARI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) kwa kushirikiana na Mamlaka za Maji Nchini Uholanzi (VEi), Leo imefanya zoezi maalumu la kutambulisha na kuzindua Maji Club katika Shule ya Sekondari Mkwakwani, ikiwa na jumla ya wanachama 100.

Zoezi hili linalenga kuendelea kuimarisha ufahamu na uelewa wa huduma zinazotolewa na Tanga UWASA kwa jamii ili kusaidia katika kufanikisha upatikanaji wa huduma ya uhakika na kupambana na maji yanayopotea (NRW).

Katika utambulisho huo, wanafunzi walipata fursa ya kueleza uelewa wao kuhusu Tanga UWASA, huku wakipewa elimu kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, kutumia maji kwa umakini, umuhimu wa kulinda miundombinu ya huduma pamoja na umuhimu wa kushiriki katika kutoa taarifa na mirejesho juu ya huduma zinazotolewa na taasisi.

Kupitia Maji Club, wanachama wanatarajiwa kuwa mabalozi wa matumizi  sahihi ya huduma za Tanga UWASA na kuhamasisha wanafunzi wenzao pamoja na jamii kuhusu umuhimu wa maji safi na salama. Aidha, club hizo zitatoa fursa kwa wanafunzi kujenga uelewa, ujuzi na uwezo wa kushiriki katika shughuli zinazolenga kuhifadhi na kulinda rasilimali za maji.

Tanga UWASA inaamini kuwa elimu kwa kizazi cha vijana ni msingi muhimu katika kujenga jamii inayothamini, inalinda na kutumia rasilimali za maji kwa uwajibikaji.