UTEKELEZAJI MRADI WA HATIFUNGANI WAFIKIA 65%
Mamlaka ya Majisaafi na usafi wa mazingira Tanga (Tang UWASA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuboresha hali ya upatikanaji huduma ya maji Tanga awamu ya tatu kupitia ufadhili wa Hatifungani ya Kijani, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 65.
Utekelezaji wa mradi huo unahusisha ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita Milioni 35, Upanuzi wa kituo cha kusukuma maji Mabayani kutoka lita Milioni 42 zilizopo sasa hadi kufikia lita Milioni 72 kwa siku, kuongeza uwezo wa kuzalisha maji katika kituo cha kutibu na kuzalisha maji cha Mowe kutoka lita Milioni 45 zilizopo sasa hadi kufikia lita Milioni 60 kwa siku, Kuongeza mtandao wa mabomba (Line extension) kwa urefu wa kilomita 60 ili kusogeza huduma karibu na wananchi kwa maeneo ambayao hayajafikiwa na huduma pamoja na kukarabati mtandao wa mabomba chakavu kwa urefu wa kilomita 110 ili kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma ya uhakika kwa wananchi.
Kukamilika kwa mradi huu mapema mwaka huu kunaenda kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi zaidi ya 555,313.62 katika Jiji la Tanga, na Miji ya Muheza, Pangani na Mkinga.

