Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

MAMLAKA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA TANGA

(Tanga UWASA)

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
/ News

TANGA UWASA YATETA NA MADIWANI - MAENDELEO YA UPATIKANAJI HUDUMA JIJINI TANGA

Imewekwa: 06 February, 2026
TANGA UWASA YATETA NA MADIWANI - MAENDELEO YA UPATIKANAJI HUDUMA JIJINI TANGA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TangaUWASA) imekutana na Waheshimiwa Madiwani kupitia kikao cha wadau kilichofanyika Februari 5, 2026 kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya upatikanaji Huduma kwa eneo la kihuduma la Tanga Jiji, ambapo Kabla ya kikao hicho, Viongizi walipata fursa ya kutembelea na kujionea maendeleo ya utekelezaji mradi wa Hatifungani katika eneo la Mowe.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mhandisi Geofrey Hilly alisema, kwa sasa kuna changamoto katika upatikanaji huduma hususani huduma ya majisafi lakini kupitia utekelezaji wa mradi wa Hatifungani huduma itaimarika na kuwa ya uhakika kwa kuwa mradi umelenga kuongeza uwezo wa uzalishaji na usambazaji wa maji kutoka mita za ujazo 45,000 kwa siku zilizopo sasa hadi kufikia mita za ujazo 60,000, Ulazaji wa mabomba makubwa ya kusukuma maji yenye kipenyo cha 600mm, Ujenzi wa tangi kubwa la kuhifadhi maji lenye mita za ujazo 35,000, Ukarabati wa mabomba chakavu, Uendelezaji wa mtandao kwa maeneo ya pembezoni, ufungaji wa Mita 10,000 za malipo kabla, kuimarisha utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji, hivyo kuimarisha upatikanaji Huduma ya uhakika kwa saa 24 na mradi unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Juni, 2026.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TangaUWASA, Dk. Fungo Ali Fungo, alisema kikao hicho ni mwanzo mzuri wa ushirikiano wa karibu kati ya Mamlaka na Madiwani, akisisitiza kuwa mikutano hiyo itakuwa ni utaratibu wa kawaida ili kuimarisha mawasiliano na uhusiano Kati ya taasisi na wadau wake muhimu.

“Tutakutana mara kwa mara kwa kuwa Madiwani ni kiungo muhimu kati yetu na wananchi, Maswali mengi ya wananchi huanzia kwenu hivyo ni muhimu kuwa na majadiliano ya karibu juu ya hali ya huduma” alisema Dk. Fungo.

Aliongeza kuwa kikao hicho kimelenga pia kuwajengea Madiwani uelewa wa kazi zinazotekelezwa na TangaUWASA ili kuwa na uelewa wa pamoja na ufahamu mzuri wa yote yanayoendelea katika kufanikisha adhma ya Serikali ya upatikanaji wa huduma ya uhakika kwa wananchi.

Nae kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Selebosi Mustafa, aliipongeza TangaUWASA kwa kuandaa kikao hicho mapema baada ya madiwani kuapishwa, akisema ni mfano mzuri wa taasisi kujenga uelewa na kuimarisha ushirikiano na viongozi wa wananchi.

Alisema lengo ni kujenga uhusiano, kuimarisha uwakilishi wa Mamlaka kwa wananchi na kuwapa madiwani nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kusimamia huduma za maji. Aidha, alishauri TangaUWASA kupanga muda wa kutosha kwa ajili ya madiwani kutembelea miradi yote ya maji na vyanzo vyake ili kujionea hali halisi ya kazi zinazotekelezwa.

Katika kikao hicho, Waheshimiwa Madiwani walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni mbalimbali yaliyojibiwa na Mhandisi Geofrey Hilly kwa kushirikiana na wataalamu wa TangaUWASA.