Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

MAMLAKA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA TANGA

(Tanga UWASA)

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
/ News

RAS TANGA ASISITIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUBORESHA UTOAJI HUDUMA NA KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJI

Imewekwa: 04 August, 2026
RAS TANGA ASISITIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUBORESHA UTOAJI HUDUMA NA KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJI

Tanga, Tanzania
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Wakurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Sekta ya Maji nchini kinacholenga kuwawezesha Wakurugenzi na Mameneja hao kubadilishana uzoefu na kujadiliana mbinu mbalimbali za kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Mchatta ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Maji kwa kuendelea kutekeleza miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuboresha upatikanaji wa huduma bora za maji nchini na kuwataka washiriki kutumia kikamilifu fursa hiyo kujifunza mbinu mpya na kubadilishana uzoefu katika utoaji wa huduma bora kwa wateja.

“Ninaamini mafunzo haya yatakuwa chachu ya kuboresha ufanisi mtakaporudi katika vituo vyenu vya kazi na hivyo kuongeza ubora wa huduma mnazozitoa kwa wananchi hususani kupitia matumizi mazuri ya tehama ,” alisema Mchatta

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi  Abbas Muslim Pyarali ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Maji amesema kikao hicho kitakachodumu kwa siku tatu kinawapa washiriki nafasi ya kupata mafunzo maalumu na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya tehama na ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Maji za kuhakikisha huduma za maji safi na usafi wa mazingira zinaendelea kuboreshwa nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka za Maji nchini, Bwana Alawi Ahmad, amesema jukwaa hilo linalotimiza miaka 10 sasa ni sehemu muhimu kwa kuwa linawapa nafasi Wakurugenzi na Mameneja kukutana, kujadiliana na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utoaji wa huduma kwa wateja na pia linatumika kama sauti ya pamoja ya Wataalamu wa huduma kwa wateja katika sekta ya maji nchini.

Wakurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Sekta ya Maji nchini wamekutana Mkoani Tanga kwa kikao kazi maalum kinachoongozwa na kaulimbiu isemayo “Huduma Janja: Matumizi ya Teknolojia kwa Huduma Bora kwa Wateja.