Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

MAMLAKA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA TANGA

(Tanga UWASA)

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
/ News

WAKURUGENZI WA HUDUMA KWA WATEJA WAVUTIWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA HATIFUNGANI

Imewekwa: 07 August, 2026
WAKURUGENZI WA HUDUMA KWA WATEJA WAVUTIWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA HATIFUNGANI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) imepokea ugeni wa Wakurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Sekta ya maji Nchini waliotembelea kujifunza na kujionea  utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Hali ya Upatikanaji wa Huduma ya Maji Tanga Awamu ya Tatu kupitia ufadhili wa Hatifungani ya Kijani ambao umefikia asilimia 72 ya utekelezaji wake.

Katika ziara hiyo, wakurugenzi hao walipata fursa ya kutembelea eneo la utekelezaji wa mradi katika Mtambo wa Kutibu na kuzalisha maji wa Mowe (Pande) na kujionea maendeleo ya upanuzi  wa miundombinu katika Mtambo wa Mowe unaolenga kuongeza uwezo wa uzalishaji maji kutoka Lita Milioni 45 kwa siku hadi kufikia Lita Milioni 60 kwa siku pamoja na ujenzi wa Tanki kubwa la kuhifadhia maji lenye ujazo wa Lita Milioni 35 na kuainishiwa namna uwekezaji huo unavyoendelenga kuongeza ufanisi wa Tanga UWASA katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ziara hiyo imefanyika kufuatia kuhitimishwa kwa kikao kazi cha Wakurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Sekta ya Maji Nchini kilichofanyika kwa siku tatu Jijini Tanga kuanzia tarehe 3 hadi 5 Agosti. Kikao hicho kilitoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kujadili mikakati ya kuboresha huduma kwa wateja na kuimarisha ushirikiano baina ya mamlaka mbalimbali za maji nchini.