DC PANGANI AKABIDHI MRADI WA VYOO SHULE YA MSINGI FUNGUNI

Imewekwa: Jul, 27 2023


Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Bi Zainab Abdallah katika ziara yake ya "Twende na Samia kijiji kwa kijiji" amekabidhi mradi wa vyoo kwa uongozi wa shule ya msingi Funguni ili vianze kutumika rasmi baada ya kuwa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia100 ili kuondokana na adha ya uhaba wa matundu ya vyoo katika shule hiyo.
"Nawashukuru na kuwapongeza wenzetu wa TANGA UWASA kwa kukamilisha utekelezaji wa mradi huu ambao unaenda kuondoa changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi wetu katika shule hii, kimsingi hii ni hatua kubwa sana na muhimu kwetu na niwaombe tusimamie na kutumia vyema miundombinu yetu" alisema DC Zainab.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANGA UWASA, Eng. Geofrey Hilly wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo amesema, " Hii ni sehemu tu ya Mradi mkubwa wa Ujenzi wa kituo cha kupokea na kutibu tope kinyesi Mjini Pangani, ambapo mradi huo unasehemu kuu tatu zinazohusisha ujenzi wa miundombinu ya kupokea na kuchakata majitaka eneo la Kumba Mtoni ambapo kazi yake imefikia asilimia 92, Ujenzi wa vyoo katika maeneo matatu ikiwemo shule ya msingi na sekondari Funguni (100%) pamoja na kituo cha mabasi Mjini Pangani (98%) na Manunuzi ya magari mawili ya usimamizi wa mradi na Gari ya Kunyonya na kusafirisha majitaka (100%). Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi M/S PERNTELS COMPANY. Ltd kwa gharama ya TZS. 998,545,461.56 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2023.
Hivyo kwakuwa ujenzi wa vyoo katika shule hii umekamilika kwa asilimia 100 na kuna uhitaji tunaomba ukabidhi miundombinu hii kwa uongozi wa shule ili vianza kutumika na wananfunzi wakati tunaendelea na ukamilishaji wa sehemu nyingine ya mradi iliyobaki, alisema Eng. Hilly
Nae Mkuu wa Shule ya Msingi Funguni Bi. Flora ameshukuru na kupokea miundombinu hiyo ambayo inaenda kusaidia sana Wananfunzi kusoma katika mazingira mazuri kwani walikuwa wakipitia changamoto kwa muda.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani katika ziara yake hiyo ameambatana pia na kamati ya Siasa Wilaya ambapo lengo kuu ni kukagua na kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika Wilaya ya Pangani.




MWISHO.