Tanga UWASA yaainisha Mikakati kukabiliana na mvua za El- Nino
Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) ikiwakilishwa na wataalamu Mha. Elikana Kayungilo kutoka Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira na Bw. Tito Lukanya kutoka Idara ya Huduma kwa Wateja imeendelea na zoezi la kutoa elimu kwa umma juu ya mikakati ya taasisi katika kukabiliana na athari za mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha kulingana na taarifa zinazoendelea kutolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na Tanga UWASA.
Wakizungumza na wananchi na wadau mbalimbali kupitia redio ya Tanga kunani (TK Fm 88.5) wataalam hao wameainisha kuwa Tanga UWASA imejipanga kwa kuwa na akiba ya Madawa ya kutosha kwa ajili ya kutibu na kusafisha maji endapo kutatokea changamoto ya upatikanaji wa dawa, kukagua na kuboresha miundombinu katika maeneo yote ya kihuduma, kusafisha mtandao wa majitaka ili kuhakikisha miundombinu inafanya kazi kwa ufanisi, pamoja na kuandaa magari yatayotumika kunyonyea majitaka endapo kutakuwa na mkwamo, pamoja na ununuzi wa pampu mpya ya kusukuma majitaka katika kituo cha Makorora ili kuongeza ufanisi wa kazi sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa wateja juu umuhimu wa kutoa taarifa za hali ya huduma katika maeneo yao kwa kutumia njia sahihi za mawasiliano za taasisi ili kuhakikisha kuwa matatizo yote yanashugulikiwa kwa wakati na huduma zinapatikana kwa ufanisi unaotakiwa.
Sambamba na hilo wataalamu hao walitumia fursa hiyo kuwahimiza wateja waliositishiwa huduma kuwa taasisi imetoa ofa ya kurejeshewa huduma bila tozo kwa kipindi cha siku 10 kuanzia tarehe 06 mpaka 16 Oktoba, 2026 hivyo wafike katika ofisi za Tanga UWASA zilizopo karibu nao kupata utaratibu wa kurejeshewa huduma.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka huu 2026 yanabebwa na kauli mbiu isemayo "The Extra Mile"

