Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji

MAMLAKA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA TANGA

(Tanga UWASA)

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
/ News

SHULE 6 ZA TANGA JIJI KUNUFAIKA NA MRADI WA SCHOOL WaSH

Imewekwa: 23 October, 2026
SHULE 6 ZA TANGA JIJI KUNUFAIKA NA MRADI WA SCHOOL WaSH

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA), kwa ufadhili wa Rotary Club ya Uholanzi na chini ya usimamizi wa VEi, imefanya kikao na wadau wa elimu ya msingi Jijini Tanga kwa lengo la kutambulisha na kujadili utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule sita za msingi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa VEi kwa kushirikiana na Tanga UWASA, Mhandisi Violet Kazumba, alisema mradi huo unalenga kuboresha miundombinu ya usafi wa mazingira na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za vyoo katika shule za msingi za Machui, Saruji, Kwanjeka, Kwakaeza, Magaoni na Mwakidila.

Alieleza kuwa shule hizo zina jumla ya wanafunzi 6,972 pamoja na walimu na watumishi 149. Kupitia mradi huo, jumla ya matundu 66 ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi, walimu na watu wenye ulemavu, pamoja na vituo 12 vya kunawia mikono yatajengwa. Mradi huo unatarajiwa kuanza Novemba 2026 na kukamilika Aprili 30, 2027, kwa gharama ya shilingi milioni 436.

Kwa upande wake, Afisa Elimu ya Msingi wa Jiji la Tanga, Mwalimu Shomari Bane, alisema mradi wa SCHOOL WaSH utasaidia Halmashauri ya Jiji la Tanga kupunguza uhaba wa matundu ya vyoo shuleni na kuchangia kufikia lengo la ujenzi wa matundu 10,000, ili kuboresha uwiano wa matumizi ya vyoo kwa wanafunzi, kwa wastani wa tundu moja kwa wasichana 20 na tundu moja kwa wavulana 25.

Aliongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu hiyo utasaidia kuweka mazingira salama na rafiki ya kujifunzia, hivyo kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu. Aidha, aliwataka wakuu wa shule zitakazonufaika na wenyeviti wa serikali za mitaa kutoa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi na kuhakikisha miundombinu itakayojengwa inatunzwa na kusimamiwa ipasavyo.

Mbali na ujenzi wa vyoo na vituo vya kunawia mikono, shule hizo zitafaidika na uboreshaji wa miundombinu ya huduma ya majisafi utakaotekelezwa na Tanga UWASA, pamoja na kufungiwa matangi ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita 5,000 kwa kila shule.

Mradi huu ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za maji, usafi wa mazingira na afya shuleni, kwa lengo la kujenga mazingira bora ya kujifunzia na kuimarisha ustawi wa wanafunzi na jamii kwa ujumla.