“Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) ni taasisi ya umma nchini iliyo chini ya Wizara ya Maji na shughuli zake zinasimamiwa na EWURA kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 05 ya mwaka 2019 pamoja na Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998, Tanga UWASA imeendelea kujidhatiti katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na za kuaminika za maji safi na usafi wa mazingira.
Dhamira ya Mamlaka Kutoa huduma bora ya majisafi na usafi wa mazingira katika eneo la huduma kwa njia inayokubalika kimazingira na kwa kutumia watumishi wenye ari ya kazi na dhima ya kumjali mteja na Dira yetu ni Kuwa Mamlaka ya kiwango cha kimataifa katika kumjali mteja kwenye utoaji wa huduma za usambazaji majisafi na usafi wa mazingira. Mamlaka imekuwa ikifanya vizuri katika utendaji wake hivyo kupata Cheti cha ubora (ISO 9001) na kuthibitishwa upya mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na uthibitisho wa ISO 9001:2015 mwaka 2022. Aidha, Tanga UWASA imeendelea kupata ripoti safi za ukaguzi na kutambuliwa na EWURA kama moja ya taasisi sita bora za maji nchini Tanzania.
Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, ninatoa shukrani za dhati kwa Serikali, washirika wa maendeleo, wadau mbalimbali na wananchi wa maeneo yanayohudumiwa na Tanga UWASA kwa ushirikiano wao wa dhati. Ushirikiano huu ni nguzo muhimu inayoiwezesha Mamlaka kufanikisha malengo yake ya kimkakati na kuendelea kutoa huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira kwa jamii.
Karibuni sana katika tovuti hii kujipatia taarifa muhimu kuhusu huduma za Tanga UWASA.”